Saturday 31 May 2014

FAMILIA YA JAMES MWAISUMBE IRINGA NA MBEYA ,INAMKUMBUKA MAMA YAO MPENDWA GRINA JAMES MWAISUMBE NI MWAKA MMOJA SASA

Familia ya James Mwaisumbe ya Iringa na Mbeya inapenda  kuwashukuru  wote  walioshiriki mazishi ya mama yao mpendwa na pia  wale  wote  wanaoendelea  kuelekeza maombi yao kwa famili  hii.

Ikumbukwe ni Tarehe 1/6/2013 ndipo mpendwa  wetu Grina James Mwaisumbe alipotutoka hapa duniani na  sasa  kesho  jumapili anafunga mwaka mmoja toka alipotutoka ,hivyo familia inaendelea kumwombea na kumkumbuka  kutokana  na ucheshi wake na ukarim na upendo mkubwa alioonyesha enzi  za uwepo  wake hapa duniani.

Grina anaendelea  kukumbukwa na mume  wake mpendwa mchungaji James Mwaisumbe ,watoto Frank ,Mpeli ,Tukuswiga,Neema, Anna na  wajukuu zako wote pamoja na ukoo wote wa akina Mwaisumbe na Msika popote  walipo.

Tunaendelea  kuamini  kuwa tulikupenda  sana na ulitupenda  zaidi ila Mungu muweza wa  yote amekupenda  zaidi yetu  hivyo hatuna budi kuendelea kukuombea kwa Mungu .

Zaidi tutaendelea kuenzi yale  yote  uliyoonyesha  enzi za uhai  wake  ikiwa ni pamoja na kuishi vema na  watu .

Bwana alitoa na Bwana ametwaha  jina lake na lihimidiwe  milele  Yote
Amina

Thursday 29 May 2014

SERIKALI KUENDELEA KUWATHAMINI WAZEE NCHINI




Na Eleuteri Mangi
Uzee na kuzeeka ni dhana inayoelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana hadi kufika hatua ya mwisho ya makuzi ambayo ni uzee. 
Binadamu ni miongoni mwa viumbe hai ambao hupitia hatua hizo katika makuzi yake, mwanasikolojia Erick Erickson aliyeishi kati ya miaka ya 1902-1994 amebaisha kuwa binadamu hupita hatua nane za makuzi hayo ikiwemo hatua ya uzee.
Kulingana na Erickson, Uzee ni hatua ya nane na ya mwisho katika maisha ya mwanadamu, hatua ambayo umri wake unaanzia na miaka 65 na kuendelea amabapo hutawaliwa kwa hekima, busara na kupungukiwa na nguvu za kufanya kazi ngumu kupita uwezo wao.
Katika nchi zilizoendelea kama Uingereza na Marekani, suala la uzee linahusishwa na umri wa kustaafu ambao ni miaka 65.
Katika nchi nyingine umri wa kustaafu unatofautiana kijinsi, kwa mfano, nchini Latvia wanaume wanastaafu wakiwa na miaka 55 wakati wanawake wanastaafu wakiwa na umri wa miaka 60. 
Hapa Tanzania mtu anaitwa mzee kutokana na ama umri mkubwa, majukumu aliyonayo na pia hadhi yake, kwa mfano mkuu mahali pa kazi au katika ukoo. 
Mwandishi wa makala haya anatumia dhana ya wazee tulionao katika nchi yetu kuwa aidha walikuwa wanafanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri au ni wale walioko vijijini ambao kuzeeka kwao ni matokeo ya kupungukiwa nguvu za kufanya kazi. 
Tanzania pamoja na ukweli kwamba watumishi walio katika Serikali na Taasisi zake wanastaafu wanapofikia miaka 60 na kwamba wazee wa vijijini na wale waliojiajiri wanakoma kufanya kazi kutokana na kuishiwa nguvu, ukweli unabaki kwamba binadamu mwenye umri wa miaka 60 anaonyesha dalili za hatua hiyo.
Kama mataifa ya dunia hii, Tanzania inajali na kutambua umuhimu wa wazee ikiamini kuwa wao ni kisima cha hekima na busara katika Maisha ya kijamii na taifa.
Ni ukweli usiopingika kuwa “wazee ni hazina”, jambo ambalo linatuaminisha palipo na wazee haliharibiki jambo kwani wao ni rasilimali na ni hazina kubwa ya maendeleo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua umuhimu wa wazee amekuwa na desturi ya kuwatumia mara kwa mara katika kutekeleza majukumu yake kitaifa na kimataifa.
Rais Kikwete anamini juu ya usemi wa “wazee ni hazina” na amekuwa akiongea nao kila anapoona ni muda muafaka kufanya hivyo.
Ipo mifano hai ya Rais Kikwete alipozungumza na wazee hao ikiwemo Mei 03, 2010 aliongea na wazee wa mkoa wa Dar es salaam juu ya mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya uchumi uliofanyika nchini Mei 05 hadi 07, 2010.
Mwaka huo huo aliongea na wazee wa Dar es salaam mnamo Julai 30, 2010 ambapo mara hii Rais Kikwete alikutana Ikulu na wazee wakongwe wa kivita nchini na wanachama wa Tanzania Legion and Club kuhusu masuala yao ikikumbukwa kuwa wazee hawa walilitumikia taifa lao kwa  umahiri mkubwa. 
Wazee hawa vili vile ni washauri wakuu na walinda amani. Hali hii inadhihirika kunapotokea migogoro mabilimbali katika jamii nyingi ambapo wazee hutumika kama hatua za awaali katika kusuluhisha na hatimaye kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo.
Kwa kuwajali, kuwalinda na kuwathamini, Umoja wa Mataifa umetenga siku ya tarehe Oktoba Mosi ya kila mwaka kuwa ni Siku ya Wazee Duniani.
Siku hii imetengwa kufuatia uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wazee katika azimio Na.46 la mwaka 1991. 
Nafasi hii imetengwa ili kuyawezesha mataifa kutafakari nafasi ya wazee katika jamii kwa kuzingatia mahitaji, matatizo na ushiriki wao katika maisha ya kila siku.  
Tanzania ambayo ni nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, imekuwa ikiadhimisha siku hii kitaifa kila mwaka ambapo mwaka huu ilifanyikia wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Kwa kawaida siku ya Wazee Duniani huadhimishwa kwa kuzingatia ujumbe maalumu wa mwaka ambao ni dira na kichicheo chenye dhana ya uhamasishaji kwa wananchi.
Lengo kubwa ni kuwawezesha kupata ufahamu na hatimaye kuweka mikakati ya utekelezaji wa masuala muhimu yaliyoamuliwa Kitaifa na Kimataifa.
Maadhimisho ya mwaka jana yaliongozwa na kauli mbiu iliyotafsiriwa na wazee wenyewe iliyosema “Matarajio ya Wazee ni Heshima, Usalama na Maisha Bora” tafsiri waliyoitoa kutoka kauli mbiu iliyotolewa na Umoja wa Mataifa “The future we want: what elder persons are saying”.
Kama taifa hatunabudi kujikumbusha na kutafakari maneno ya busara yaliyotamkwa na aliyekuwa Kaibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Anan, “Huwezi kufurahia usalama bila maendeleo, hatuwezi kufurahia maendeleo bila usalama na hatuwezi kufurahia hivyo vyote bila kuheshimu haki za binadamu”
Katika kuadhimisha siku ya Wazee Duniani, kuna mambo ambayo Tanzania kama taifa imefanya juhudi na itaendelea kufanyia kazi kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyojieleza.
Nchi yetu imekuwa ikizingatia misingi ya sheria na utawala bora na hivyo kudumisha amani, heshima na kujali maisha ya watu wake. 
Katika kuadhimisha siku ya Wazee Duniani mwaka huu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilal, alisema kuwa nia ya Serikali ya kupambana na vitendo vya uvunjifu wa amani katika nchi yetu bado ipo palepale.
Dkt. Bilal alisisitiza, “Nawasihi Watanzania wote tushirikiane bega kwa bega na Serikali katika kujenga, kulinda na kudumisha amani kwa wazee”. 
Katika kuadhimisha Mwaka wa Kimataifa wa Wazee (1999) Serikali ilifanya maamuzi ya kuwa na Sera ya Taifa ya Wazee. 
Maamuzi ya kuwa na Sera hii ni kielelezo cha dhamira hai na dhati ya Serikali ya kuweka masuala ya wazee katika agenda ya maendeleo ya nchi yetu. 
Serikali inatambua kwamba wazee wetu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na umaskini, kutotosheleza kwa huduma za afya, pensheni na kutoshirikishwa katika maamuzi muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi yao.  
Pamoja na hali hii, Serikali inatambua kwamba wazee ni raslimali na nguvu mpya katika maendeleo ya nchi. Jitihada zitaendelea kuwekwa kuhakikisha kwamba wazee wanatambuliwa na wanapata fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi yao sanjari na wananchi wengine. 
Kuwapo kwa Sera ya Taifa ya Wazee ni hatua ngeni kwa nchi nyingi, Tanzania ikiwa moja wapo.
Katika bara la Afrika, Tanzania imekuwa nchi ya pili kuwa na Sera ya aina hii baada ya Mauritius. Endapo kutatokea upungufu katika matamko na utekelezaji wa Sera yenyewe Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itakuwa tayari kufanya marekebisho pale yanapohitajika. 
Kwa Serikali, watumishi wa umma na jamii nzima, Sera ya wazee kwa taifa letu ni mwongozo katika kuandaa mipango, utekelezaji na tathmini utoaji huduma kwa wazee. 
Hivyo, Serikali itaendelea kuwaenzi wazee wetu kwa heshima, usalama na maisha bora suala ambalo ni msingi na nguzo kwa maendeleo yetu. Maisha bora yatakuja kama tutawawezesha makundi maalumu katika jamii wakiwemo wazee. 
Kwa kupitia takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa kuhusu sense ya watu na makazi iliyofanyika Agosti 26, 2012 zinaonesha kuwa kuna jumla ya wazee Tanzania ni 2,507,568 sawa na asilimia 5.6 ya Watanzania wote.
Jumla hii inaundwa na wazee wanakiume 1,200,210 sawa na asilimia 5.5 na wanakike 1, 307, 358 sawa na asilimia 5.7 
Tofauti na sense ya watu na makazi ya mwaka 2002 ambapo wazee wazee walikuwa asilimia 4.0
Tasira hii inaonesha kuwa idadi ya wazee nchini imeongezeka kwa tofauti ya asilimia 1.6, tofauti hii inaonesha taswira na mwelekeo kuwa kuwa idadi ya wazee chini wataendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Itakumbukwa kuwa tangu mwaka 2002, Tanzania ilipoungana na mataifa mengine duniani kutia saini ya Mkataba wa Kimataifa wa wazee ilikuwa ni kielelezo tosha cha kuwathamini wazee na hivyo kuanza kubuni, kuweka mipango mbalimbali yenye lengo la kuboresha maisha yao
Katika maadhimisho siku ya Wazee Duniani mwaka huu, Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Seif S. Rashid, ametaja kuwa baadhi ya mipango ambayo Serikali imetekeleza ni pamoja na kuwepo kwa Sera ya Taifa ya Wazee iliyotungwa 2003 kwa ajili ya kusimamia mipango na mikakati mbalimbali inayolenga wazee na hivyo kutambuliwa kwao kama kundi pekee na ushiriki wao katika mipango ya maendeleo ya taifa. 
Naibu Waziri Rashid alikiri na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za hari, hii ni katika hatua ya kuboresha huduma zitolewazo katika makazi 41 yanayowatunza wazee wenye shida na wasiona ndugu wa kuwatunza hapa nchini.
Akitoa msimamo wa Serikali Naibu Waziri alisema, “Thamani ya mchango wa wazee inatambuliwa na Serikali hasa inapoendelea kuboresha utaratibu wa utoaji matibabu kwa wazee wote bila malipo”.
Eneo hili linaendelea kuboreshwa ili huduma kwa wazee zitolewe bila vikwazo vyovyote.
Kwa kuzingatia Waraka wa Serikali uliotolewa Februari mosi, 2007, Serikali imetoa msamaha wa kodi ya majengo wanayoishi wazee na yasiyokuwa ya biashara.
Ili kulinda usalama wa wazee, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeendelea kuchukuahatua kali za kisheria kwa wale wote wanaobainika kujihusisha na mauaji ya wazee.
Vile vile, Serikali itaendelea kuelimisha jamii juu ya madhara yatokanayo na vitendo viovu dhidi ya wazee.
Kwa kutambua mchango mkubwa na umuhimu wa wazee, Serikali imewashirikisha wazee katika kutoa maoni yao katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu masuala yao.
Katika kuwaenzi wazee, ni dhahiri kama taifa litaendelea kunufaika na michango yao, hivyo hatuna budi kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuishi ili waendelee kuchangia katika maendeleo ya taifa. 
Kuwepo kwa taifa lenye amani ni matokeo ya misingi mizuri walioijenga wazee wetu tangu hapo awali kwa kuwajali, kuwaenzi watu wote bila kujali umri na hali zao za maisha katika hatua mbalimbali kama zilivyoainishwa na Mwanasikolojia Erick Erickson. 
Mwisho

Tuesday 27 May 2014

SAMAHANI KWA PICHA: MAJAMBAZI DAR WAUA POLISI KINYAMA, NAO WAUAWA NA WANANCHI WENYE HASIRA.....


 Mwili wa askari aliyeuawa ukiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Temeke

Askari polisi mmoja wa kituo cha polisi Chang'ombe, Mkoa wa kipolisi wa Temeke, ameuawa kikatili siku ya ijumaa mchana baada ya kupigwa risasi ya kifua na majambazi waliokuwa wanajaribu kutoroka baada ya kufanya tukio la kihalifu. Askari hao waliokuwa doria katika eneo la Wailes walijikuta wakishambuliwa kwa risasi na majambazi hao mara baada ya majambazi hao kujaribu kukimbia katika eneo la tukio kwa kutumia usafiri wa pikipiki kipindi ambapo askari polisi walikuwa karibu na eneo la tukio. Hata hivyo wakati askari hao wakijaribu kuwafukuza majambazi hao wawili kwa lengo la kuwakamata ndipo jambazi mmoja alitoa bastola na kumpiga risasi ya kifua askari huyo na kufariki pale pale.
Mwili wa askari huyo ukiwa umehifadhiwa.


Hata hivyo katika harakati za kujaribu kukimbia majambazi hao walianguka na pikipiki waliyokuwa wakitumia ndipo wakaamua kutimua mbio mitaani na kuingia katika nyumba moja ambapo walijificha na kujifanya kama ni wakazi wa eneo hilo, baada ya wnanchi na polisi kufika katika nyumba hiyo, baadhi ya majirani waliwaambia polisi kwamba wameona watu hao wameingia katika nyumba hiyo. Baada ya polisi kuingia waliwakuta watu hao wakiwa wametulia kama kwamba wao ni wakaazi wa nyumba hiyo na wala hawajui lililotokea.
Mwili wa mmoja wa majambazi ukiwa chumba cha kuhifadhia maiti

Baada ya kuwatambua watu hao, polisi waliwatia nguvuni huku wananchi wenye ghadhabu waking'ang'ania kuwa wanataka kuwaua sababu wameshaua askari mmoja. Baada ya vuta nikuvute kati ya wananchi na askari hao ambao walikuwa wachache, wananchi walifanikiwa kuwachukua majambazi hao kwa nguvu kutoka mikononi mwa polisi na kuanza kuwapiga kwa silaha mbalimbali za kienyeji yakiwemo mawe na marungu mpaka watuhumiwa hao wakapoteza maisha.
Mwili wa jambazi mwingine ukiwa umeharibika vibaya baada ya kipigo kikali kutoka kwa wananchi wenye hasira.
Mwili wa askari polisi ukiwa umepakiwa kwenye gari ya polisi tayari kupelekwa hospitali ya Temeke kuhifadhiwa.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo waliiambia blogu hii kwamba majambazi hayo kabla ya kupambana na polisi walikuwa wamefanya uvamizi na kumuibia mwanamke mmoja mkazi wa eneo hilo. Hata hivyo mali au fedha iliyoibiwa haikuweza kujulikana mara moja.

Monday 26 May 2014

TUNDU LISU AWATAJA MAWAZIRI,WABUNGE WALIOOMBAFEDHA


 



Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amewataja kwa majina mawaziri na wabunge aliosema bungeni kuwa wamekuwa ombaomba katika mifuko ya hifadhi ya jamii.
 
Baadhi ya waliotajwa ni pamoja na Mbunge wa Kongwa ambaye pia ni Naibu Spika, Job Ndugai; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi; Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana na wabunge Betty Machangu (Viti Maalumu), Livingstone Lusinde (Mtera), John Komba (Mbinga Magharibi), Eugen Mwaiposa (Ukonga) na Gudluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi).
 
Hata hivyo, gazeti hili halijawataja majina mawaziri na wabunge wengine waliomo kwenye orodha hiyo ya Lissu kwa kuwa hawakupatikana jana kujibu tuhuma hizo.


Mbali na kuwataja kwa majina, Lissu pia ametoa vielelezo vinavyoonyesha jinsi walivyokuwa wakiidhinishiwa malipo kwa nyakati tofauti na Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (LAPF), kwa sababu mbalimbali.
 
Lissu alimwambia mwandishi wetu jana kuwa licha ya kiwango cha fedha kutokuwa kikubwa, lakini kinaweza kusababisha mgongano wa kimasilahi kati ya wajibu wa wabunge kwa umma na masilahi yao binafsi.
 
"Hali hii inaweza kusababisha Bunge likashindwa kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia Serikali na taasisi zake," alisema Lissu huku akisisitiza azimio lake la kuwasilisha hoja binafsi kwa Spika wa Bunge ili iundwe tume kuchunguza suala hilo.
 
Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Eliud Sanga jana alikiri kuwa shirika hilo liliidhinisha malipo kwa mawaziri na wabunge hao kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo.
 
Hata hivyo, alisema shirika hilo halitoi fedha taslimu, bali hununua vitu ambavyo viliombwa na viongozi hao kwa ajili ya kusaidia wananchi na si kufanya biashara.
Sakata lenyewe
 
Akizungumzia jinsi mawaziri na wabunge hao walivyosaidiwa, Lissu alisema LAPF ilitoa Sh2.5 milioni kwa ajili ya mradi wa madarasa Jimbo la Kongwa linaloongozwa na Ndugai.
 
Alipoulizwa kuhusu madai hayo, Ndugai alisema hakuna tatizo lolote kwa mbunge kupewa msaada na mfuko wa kijamii.
 
"Huyo Lissu ana upungufu mkubwa. Hivi LAPF ikisaidia Sh2 milioni kwa ujenzi wa darasa unaogharimu Sh10 milioni ni tatizo hilo? Nchi hii inakwenda wapi jamani, siyo kila kitu wanachozungumza wapinzani ni hoja, kama LAPF wangekuwa wanatoa fedha lingekuwa tatizo lakini wanasaidia vifaa tu."
CHANZO:MWANANCHI

KITUO CHA NURU OPHANS CHAKABIDHI VITENDEA KAZI KWA VIJANA WANAOISHI KWENYE MAZINGIRA MAGUMU MBEYA


 Venance Matinya kutoka  mtandao wa Mbeya yetu Blog  akipokea Hati ya shukrani kutoka kwa Mgeni Rasmi Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mbeya, Thobias Mwalwego kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa kwa kutambua mchango wa Mbeya yetu  Blog katika kulea watoto yatima

 mwanafunzi aliyehitimu fani ya ufundi wa magari akikabidhiwa vifaa vyake.
 Mwanafunzi aliyehitimu fani ya kilimo cha mbaogamboga akikabidhiwa vitendea kazi.
 Mwanafunzi wa fani ya useremala naye akikabidhiwa vitendea kazi.
 Mgeni rasmi, Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Mbeya, Thobias Mwalwego akihutubia katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro.
Mwanafunzi wa fani ya ushonaji akikabidhiwa vitendea kazi ambacho ni Cherehani.
  Meneja wa Kituo, Amanda Fihavango akiwaeleza jambo waandishi wa habari
.Mkurugenzi wa Nuru Orphans centre Jasson Fihavango akisoma risala.
 Mwanafunzi akikabidhiwa cheti cha kuhitimu masomo yake.
Wageni waalikwa wakitembelea majengo ya kituo cha nuru.

KITUO cha Nuru Ophans kimekabidhi vitendea kazi kwa vijana wanaoishi kwenye mazingira magumu Mbeya baada ya kuhitimu mafunzo ya fani mbali mbali kutoka Chuo cha ufundi Veta mkoani Mbeya.
 
Hafla hiyo ilifanyika juzi katika makao makuu ya kituo hicho kilichopo Uyole Jijini Mbeya ambapo vijana 30 walipewa vyeti vya kuhitimu masomo yao pamoja na vifaa vya kufanyia kazi.
 
Meneja Miradi wa Nuru Ophans Centre, Osward Poyo,alisema Asasi yake baada ya kufanya utafiti ilibaini kuwepo kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu  2500 katika kata 6.
 
Alisema baada ya kubaini hayo Asasi hiyo iliomba msaada kwa Ubalozi wa Marekani nchini kwa ajili ya kuwasomesha vijana hao fani mbali mbali za ufundi lakini Ubalozi ulikubali kuwasomesha vijana 30 tu hivyo kufanya kila kata kutoa vijana 5.
 
Aliongeza kuwa Ubalozi wa Marekani baada ya kutiliana sahihi mkataba wa kuwasomesha vijana hao walitoa jumla ya shilingi 16,800,000 kwa malipo ya ada, Nauli ya kwenda na kurudi chuoni, malipo ya chakula kwa siku zote za masomo na ununuzi wa Vitendea kazi kulingana na fani ambazo vijana wamesomea.
 
Alizitaja fani ambazo vijana hao wamesomea na vifaa walivyokabidhiwa kuwa ni pamoja na fani ya Ushonaji ambayo ilikuwa na vijana 12 waliokabidhiwa Cherehani kila mmoja,Seremala kijana mmoja aliyekabidhiwa Misumeno 3,Landa 2, Nyundo pamoja na Ovaroli.
 
Wengine ni fani za Ufundi magari ambao ulikuwa na vijana 6 ambao kila mmoja alikabidhiwa Ovaroli,dazani ya spana na Jeki ya kuinulia magari na vijana 9 waliochukua fani ya udereva ambao walipewa Leseni za kuendeshea magari na vijana wawili waliosoma fani ya klilimo cha mboga mboga ambao walipewa kila mmoja kilo 50 za mbolea aina ya Urea, Mbegu za mahindi kilo 6, Pumpu ya kunyunyizia dawa 1 pamoja na mbegu za mboga za nyanya, spinachi na karoti.
 
Naye Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Mbeya,Thobias Mwalwego, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, alitoa wito kwa vijana wa fani za ufundi kuwa waaminifu kwa wateja wao na huduma watakazokuwa wakitoa kwa manufaa ya jamii nzima.
 
Alisema vifaa walivyokabidhiwa vinafaa kutunzwa na siyo kukimbilia kuuza hali ambayo inaweza kuwarudisha katika hali ya awali ya kuzurura mitaani bila kuwa na fani ya kufanya.

Na mwandishiwetu

MAVUNO MAKUBWA YA MAHINDI SHAMBANI KWA MHE. PINDA

PG4A0268 PG4A0291Waziri Mkuu,Mizengo Pinda  akikagua mavuno ya mahindi kutoka shmabani kwake yaliyokusanywa nyumbani kwake Kibaoni wilayani Mlele, Mpanda Mai 24, 2014. Mheshimiwa Pinda anatarajia uvuna zaidi ya magunia 1000 ingawa ekari tano za mahindi hayo ziliharibiwa na Tembo kutoka hifadhi ya katavi. (Picha na Ofisi yaWaziri Mkuu

TAJIRI MKUBWA CHINI AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA



Tajiri mmoja anayeaminika kuwa mshirika wa aliyekuwa mkuu wa ujasusi nchini China Zhou Yongkang, amehukumiwa kifo.
Mahakama imewapata na hatia Liu Han na kakake Liu Wei ya kupanga mauaji ya aina ya kimafia.

Wanaume hao walikuwa miongoni mwa kikundi cha watu 36 walioshitakiwa na makosa sawa na hayo.
Hukumu dhidi ya Liu Han inaaminika kuwa sehemu ya mpango wa serikali kupambana na ufisadi.

Mahakama ilisema kuwa Liu Han alikuwa amefaidika kifedha kutokana na vitendo vya uhalifu.
Pia katika matukio mengi walifanya mauaji na vitendo vya uhalifu ambavyo waliwadhuru watu na hata kuwazuilia watu kinyume na sheria.
Kwa mujibu wa mahakama Bwana Liu aliendesha shughuli zake kwa kusaidiwa na maafisa kadhaa wa serikali ili kuweza kudhibiti mashine za michezo katika mkoa wa Guanghan .

Liu, ambaye ni mkuu wa zamani wa kampuni ya madini ya Sichuan Hanlong Group, aliorodheshwa katika nafasi ya 148 kwa utajiri wake duniani na jarida la Forbes mwaka 2012.

Kampuni yake iliwahi kujaribu kutaka kuinunua kampuni ya madini ya Australia Sundance Resources Ltd ingawa hilo halikufanyika.
Kesi hii bila shaka inazua maswali kadhaa kwa viongozi wa kisiasa nchini China.
Huenda mkuu wa zamani wa ujasusi Zhou Yongkang pia akashitakiwa kwa kushirikiana na Liu.

Ikiwa jambo hilo litafanyika, hesi dhidi yake itakuwa ya madai mabaya zaidi ya ufisadi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya china.


Chanzo:bbc