Na Eleuteri
Mangi
Uzee na kuzeeka
ni dhana inayoelezea hatua ya mwisho ya makuzi ya binadamu kuanzia utoto, ujana
hadi kufika hatua ya mwisho ya makuzi ambayo ni uzee.
Binadamu ni miongoni
mwa viumbe hai ambao hupitia hatua hizo katika makuzi yake, mwanasikolojia
Erick Erickson aliyeishi kati ya miaka ya 1902-1994 amebaisha kuwa binadamu hupita
hatua nane za makuzi hayo ikiwemo hatua ya uzee.
Kulingana na Erickson, Uzee
ni hatua ya nane na ya mwisho katika maisha ya mwanadamu, hatua ambayo umri
wake unaanzia na miaka 65 na kuendelea amabapo hutawaliwa kwa hekima, busara na
kupungukiwa na nguvu za kufanya kazi ngumu kupita uwezo wao.
Katika nchi
zilizoendelea kama Uingereza na Marekani, suala la uzee linahusishwa na umri wa
kustaafu ambao ni miaka 65.
Katika nchi
nyingine umri wa kustaafu unatofautiana kijinsi, kwa mfano, nchini Latvia
wanaume wanastaafu wakiwa na miaka 55 wakati wanawake wanastaafu wakiwa na umri
wa miaka 60.
Hapa Tanzania
mtu anaitwa mzee kutokana na ama umri mkubwa, majukumu aliyonayo na pia hadhi
yake, kwa mfano mkuu mahali pa kazi au katika ukoo.
Mwandishi wa
makala haya anatumia dhana ya wazee tulionao katika nchi yetu kuwa aidha
walikuwa wanafanya kazi za kuajiriwa au kujiajiri au ni wale walioko vijijini
ambao kuzeeka kwao ni matokeo ya kupungukiwa nguvu za kufanya kazi.
Tanzania pamoja
na ukweli kwamba watumishi walio katika Serikali na Taasisi zake wanastaafu
wanapofikia miaka 60 na kwamba wazee wa vijijini na wale waliojiajiri wanakoma
kufanya kazi kutokana na kuishiwa nguvu, ukweli unabaki kwamba binadamu mwenye
umri wa miaka 60 anaonyesha dalili za hatua hiyo.
Kama mataifa ya dunia
hii, Tanzania inajali na kutambua umuhimu wa wazee ikiamini kuwa wao ni kisima
cha hekima na busara katika Maisha ya kijamii na taifa.
Ni ukweli usiopingika
kuwa “wazee ni hazina”, jambo ambalo linatuaminisha palipo na wazee
haliharibiki jambo kwani wao ni rasilimali na ni hazina kubwa ya maendeleo.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kutambua umuhimu wa wazee
amekuwa na desturi ya kuwatumia mara kwa mara katika kutekeleza majukumu yake
kitaifa na kimataifa.
Rais Kikwete anamini
juu ya usemi wa “wazee ni hazina” na amekuwa akiongea nao kila anapoona ni muda
muafaka kufanya hivyo.
Ipo mifano hai ya Rais Kikwete
alipozungumza na wazee hao ikiwemo Mei 03, 2010 aliongea na wazee wa mkoa wa
Dar es salaam juu ya mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya uchumi uliofanyika
nchini Mei 05 hadi 07, 2010.
Mwaka huo huo aliongea
na wazee wa Dar es salaam mnamo Julai 30, 2010 ambapo mara hii Rais Kikwete
alikutana Ikulu na wazee wakongwe wa kivita nchini na wanachama wa Tanzania
Legion and Club kuhusu masuala yao ikikumbukwa kuwa wazee hawa walilitumikia
taifa lao kwa umahiri mkubwa.
Wazee hawa vili vile ni
washauri wakuu na walinda amani. Hali hii inadhihirika kunapotokea migogoro
mabilimbali katika jamii nyingi ambapo wazee hutumika kama hatua za awaali
katika kusuluhisha na hatimaye kupata ufumbuzi wa migogoro hiyo.
Kwa kuwajali, kuwalinda
na kuwathamini, Umoja wa Mataifa umetenga siku ya tarehe Oktoba Mosi ya kila
mwaka kuwa ni Siku ya Wazee Duniani.
Siku hii imetengwa
kufuatia uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wazee katika
azimio Na.46 la mwaka 1991.
Nafasi hii imetengwa
ili kuyawezesha mataifa kutafakari nafasi ya wazee katika jamii kwa kuzingatia
mahitaji, matatizo na ushiriki wao katika maisha ya kila siku.
Tanzania ambayo ni nchi
mwanachama wa Umoja wa Mataifa, imekuwa ikiadhimisha siku hii kitaifa kila
mwaka ambapo mwaka huu ilifanyikia wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
Kwa kawaida siku ya
Wazee Duniani huadhimishwa kwa kuzingatia ujumbe maalumu wa mwaka ambao ni dira
na kichicheo chenye dhana ya uhamasishaji kwa wananchi.
Lengo kubwa ni
kuwawezesha kupata ufahamu na hatimaye kuweka mikakati ya utekelezaji wa
masuala muhimu yaliyoamuliwa Kitaifa na Kimataifa.
Maadhimisho ya mwaka
jana yaliongozwa na kauli mbiu iliyotafsiriwa na wazee wenyewe iliyosema “Matarajio
ya Wazee ni Heshima, Usalama na Maisha Bora” tafsiri waliyoitoa kutoka kauli
mbiu iliyotolewa na Umoja wa Mataifa “The future we want: what elder persons
are saying”.
Kama taifa hatunabudi
kujikumbusha na kutafakari maneno ya busara yaliyotamkwa na aliyekuwa Kaibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Anan, “Huwezi kufurahia usalama bila maendeleo,
hatuwezi kufurahia maendeleo bila usalama na hatuwezi kufurahia hivyo vyote
bila kuheshimu haki za binadamu”
Katika kuadhimisha siku
ya Wazee Duniani, kuna mambo ambayo Tanzania kama taifa imefanya juhudi na
itaendelea kufanyia kazi kama kauli mbiu ya mwaka huu inavyojieleza.
Nchi yetu imekuwa
ikizingatia misingi ya sheria na utawala bora na hivyo kudumisha amani, heshima
na kujali maisha ya watu wake.
Katika kuadhimisha siku
ya Wazee Duniani mwaka huu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Mohamed Gharib Bilal, alisema kuwa nia ya Serikali ya kupambana na vitendo
vya uvunjifu wa amani katika nchi yetu bado ipo palepale.
Dkt. Bilal alisisitiza,
“Nawasihi Watanzania wote tushirikiane bega kwa bega na Serikali katika kujenga,
kulinda na kudumisha amani kwa wazee”.
Katika kuadhimisha
Mwaka wa Kimataifa wa Wazee (1999) Serikali ilifanya maamuzi ya kuwa na Sera ya
Taifa ya Wazee.
Maamuzi ya kuwa na Sera
hii ni kielelezo cha dhamira hai na dhati ya Serikali ya kuweka masuala ya
wazee katika agenda ya maendeleo ya nchi yetu.
Serikali inatambua
kwamba wazee wetu wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na
umaskini, kutotosheleza kwa huduma za afya, pensheni na kutoshirikishwa katika
maamuzi muhimu yanayohusu maendeleo ya nchi yao.
Pamoja na hali hii,
Serikali inatambua kwamba wazee ni raslimali na nguvu mpya katika maendeleo ya
nchi. Jitihada zitaendelea kuwekwa kuhakikisha kwamba wazee wanatambuliwa na
wanapata fursa ya kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi yao sanjari na
wananchi wengine.
Kuwapo kwa Sera ya
Taifa ya Wazee ni hatua ngeni kwa nchi nyingi, Tanzania ikiwa moja wapo.
Katika bara la Afrika,
Tanzania imekuwa nchi ya pili kuwa na Sera ya aina hii baada ya Mauritius.
Endapo kutatokea upungufu katika matamko na utekelezaji wa Sera yenyewe Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii itakuwa tayari kufanya marekebisho pale yanapohitajika.
Kwa Serikali, watumishi
wa umma na jamii nzima, Sera ya wazee kwa taifa letu ni mwongozo katika kuandaa
mipango, utekelezaji na tathmini utoaji huduma kwa wazee.
Hivyo, Serikali
itaendelea kuwaenzi wazee wetu kwa heshima, usalama na maisha bora suala ambalo
ni msingi na nguzo kwa maendeleo yetu. Maisha bora yatakuja kama tutawawezesha makundi
maalumu katika jamii wakiwemo wazee.
Kwa kupitia takwimu
zilizotolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa kuhusu sense ya watu na makazi
iliyofanyika Agosti 26, 2012 zinaonesha kuwa kuna jumla ya wazee Tanzania ni 2,507,568
sawa na asilimia 5.6 ya Watanzania wote.
Jumla hii inaundwa na
wazee wanakiume 1,200,210 sawa na asilimia 5.5 na wanakike 1, 307, 358 sawa na
asilimia 5.7
Tofauti na sense ya
watu na makazi ya mwaka 2002 ambapo wazee wazee walikuwa asilimia 4.0
Tasira hii inaonesha
kuwa idadi ya wazee nchini imeongezeka kwa tofauti ya asilimia 1.6, tofauti hii
inaonesha taswira na mwelekeo kuwa kuwa idadi ya wazee chini wataendelea
kuongezeka mwaka hadi mwaka.
Itakumbukwa kuwa tangu
mwaka 2002, Tanzania ilipoungana na mataifa mengine duniani kutia saini ya
Mkataba wa Kimataifa wa wazee ilikuwa ni kielelezo tosha cha kuwathamini wazee
na hivyo kuanza kubuni, kuweka mipango mbalimbali yenye lengo la kuboresha
maisha yao
Katika maadhimisho siku
ya Wazee Duniani mwaka huu, Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa
Jamii Dkt. Seif S. Rashid, ametaja kuwa baadhi ya mipango ambayo Serikali
imetekeleza ni pamoja na kuwepo kwa Sera ya Taifa ya Wazee iliyotungwa 2003 kwa
ajili ya kusimamia mipango na mikakati mbalimbali inayolenga wazee na hivyo
kutambuliwa kwao kama kundi pekee na ushiriki wao katika mipango ya maendeleo
ya taifa.
Naibu Waziri Rashid
alikiri na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za hari,
hii ni katika hatua ya kuboresha huduma zitolewazo katika makazi 41
yanayowatunza wazee wenye shida na wasiona ndugu wa kuwatunza hapa nchini.
Akitoa msimamo wa Serikali
Naibu Waziri alisema, “Thamani ya mchango wa wazee inatambuliwa na Serikali
hasa inapoendelea kuboresha utaratibu wa utoaji matibabu kwa wazee wote bila
malipo”.
Eneo hili linaendelea
kuboreshwa ili huduma kwa wazee zitolewe bila vikwazo vyovyote.
Kwa kuzingatia Waraka
wa Serikali uliotolewa Februari mosi, 2007, Serikali imetoa msamaha wa kodi ya
majengo wanayoishi wazee na yasiyokuwa ya biashara.
Ili kulinda usalama wa
wazee, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo imeendelea kuchukuahatua
kali za kisheria kwa wale wote wanaobainika kujihusisha na mauaji ya wazee.
Vile vile, Serikali
itaendelea kuelimisha jamii juu ya madhara yatokanayo na vitendo viovu dhidi ya
wazee.
Kwa kutambua mchango
mkubwa na umuhimu wa wazee, Serikali imewashirikisha wazee katika kutoa maoni
yao katika Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu masuala
yao.
Katika kuwaenzi wazee,
ni dhahiri kama taifa litaendelea kunufaika na michango yao, hivyo hatuna budi
kuweka mazingira mazuri zaidi ya kuishi ili waendelee kuchangia katika
maendeleo ya taifa.
Kuwepo kwa taifa lenye
amani ni matokeo ya misingi mizuri walioijenga wazee wetu tangu hapo awali kwa kuwajali,
kuwaenzi watu wote bila kujali umri na hali zao za maisha katika hatua
mbalimbali kama zilivyoainishwa na Mwanasikolojia Erick Erickson.
Mwisho
No comments:
Post a Comment